Ofisa
Habari wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Florence Temba (kushoto),
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, HAB Mkwizu, Mkurugenzi
wa Idara ya Maendeleo ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, Roxana
Kijazi pamoja na meneja mafunzo wa wakala wa utumishi kwa njia ya
mtandao, Dickson Mwanyika (kulia).
MKUTANO Mkuu wa Wakuu wa Utumishi wa Umma wa Nchi za Afrika, Wanachama wa Jumuiya ya Madola, unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Julai 13-15, mwaka huu.
Mkutano huo unatarajia kufanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo unatarajiwa kuhudhuriwa na nchi wanachama 18 za Jumuiya ya Madola.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, HAB Mkwizu amezitaja nchi hizo ambazo tayari zimeridhia kushiriki mkutano huo kuwa ni Botswana, Cameroon, Ghana, Kenya, Msumbiji, Namibia, Sierra Lione, Afrika Kusini, Swaziland, Uganda na Zambia.
Alisema kuwa mkutano huo unaratibiwa kwa kushirikiana na sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ambao hufanyika kila mwaka ukiwa na lengo la kuwakutanisha wakuu wa utumishi wa umma wa nchi za Afrika ambao ni wanachama, kujadili masuala ya changamoto zinazokabili sekta ya utumishi wa umma katika nchi husika, kubadilishana uzoefu, pamoja na kuweka maazimio ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbambali ili kuimarisha utendaji na ufanisi.
Aliongeza kuwa mikutano hiyo ya wakuu wa utumishi wa umma ilianza Juni 2004 ambapo mkutano wake wa kwanza ulifanyika mjini London Uingereza na Tanzania ikipewa heshima ya nchi ya kwanza Bara la Afrika kuandaa mkutano wa pili uliofanyika mjini Arusha hivyo mkutano wa mwaka huu ukiwa wa ni awamu ya pili kufanyika nchini Tanzania.
Aidha, Mkwizu alisema kuwa Tanzania kupewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo lilifikiwa katika mkutano wa 11 uliofanyika Julai 8, 2014, Port Luis Mauritius , hivyo akaeleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu kwenye mkutano wa huo ni, ‘kutoka katika mipango mizuri iliyopo hadi kwenye ubora zaidi wa sera, mikakati, pamoja na utekelezaji wa kiwango cha juu katika huduma za kijamii.