Friday, December 26, 2014

RAY C KUFA NDANI YA SIKU 97!


Na Waandishi wetu
Staa anayetamba na ngoma mpya ya ‘Nshumu Nshumu’, Rehema Chalamila ‘Ray C’ amevamiwa na kung’atwa mguuni na paka anayesadikiwa kuwa na kichaa hivyo kuibua mjadala kuwa endapo hatazingatia chanjo (Vaccination) anahofiwa kufa ndani ya siku 97 tangu alipokutwa na kisanga hicho wiki mbili zilizopita.
Staa anayetamba na ngoma mpya ya ‘Nshumu nshumu’, Rehema Chalamila ‘Ray C’.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, Ray C aling’atwa na paka huyo eneo la kutolea dawa za Methadone, ndani ya Hospitali ya Mwananyamala, Dar ambapo alikwenda kunywa dawa ya kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.

“Ray C alikuwa anakatiza kwa miguu, ghafla akarukiwa na paka na kumng’ang’ania mguu kwa meno.
“Ray C alijaribu kumzuia lakini hakufanikiwa hivyo alisababisha bonge la tafrani. Kama siyo watu kumsaidia yule paka asingetoka mguuni kwake,” alisema shuhuda huyo akisisitiza si bure paka huyo alikuwa na kichaa (rabies).

Ilifahamika kwamba baada ya paka huyo kumvamia, alikimbilia chumba cha matibabu hospitalini hapo ambapo alipata huduma ya kwanza lakini baada ya hapo mguu wake ulianza kuvimba.Baada ya kunyetishiwa ishu hiyo, Ijumaa lilimtafuta Ray C ambaye alikiri kuvamiwa na kung’atwa na paka huyo huku akipinga madai kwamba labda alitumiwa kichawi.
“Kiukweli naendelea vizuri na jeraha limepona baada ya kupatiwa matibabu. Watu wanasema sana lakini mimi sina imani za kichawi,” alisema Ray C.Maelezo ya kitaalam yalionesha kwamba endapo Ray C aling’atwa na paka mwenye kichaa, muda wa kupata virusi vya ugonjwa huo hadi kuanza kwa dalili, kwa kawaida unaweza kuwa kati ya wiki 3 hadi 12.
‘Ray C’.
Maelezo hayo ya kitaalam yalieleza kwamba, mara baada ya kung’atwa, Ray C alipaswa kupata chanjo ya kwanza siku hiyohiyo, chanjo ya pili ilitakiwa iwe baada ya siku tatu, chanjo ya tatu iwe baada ya siku saba na chanjo ya mwisho iwe baada ya siku kumi na nne kama alikuwa hajapata chanjo hiyo kabla.
Kama Ray C aliwahi kuchanjwa dhidi ya ugonjwa huo, alipaswa apewe chanjo mbili, moja palepale (kinga) na nyingine siku ya tatu.Kitaalam ilielezwa kwamba kama Ray C hatafuata utaratibu huo wa chanjo, atakaa kati ya siku 21 hadi 90 ambapo dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa zitakuwa zimeanza kuonekana, ukijumlisha na siku saba za kuumwa basi atakiona kifo ndani ya siku 97 hivyo cha msingi ni kuzingatia chanjo.
Dalili za mtu mwenye ugonjwa huo ambao kiwango cha kuua ni asilimia 100, ni pamoja na homa kali, kuumwa kichwa, kuvimba na kuwashwa koo.
Nyingine ni kuwa mwoga, kuchanganyikiwa, kuwa na tabia zisizo za kawaida, maumivu, kuona vitu ambavyo havipo (maruweruwe), kujifichaficha kwenye kona au kukimbia, kuogopa maji (hydrophobia), mwili kupooza na  kushindwa kula. Nyingine ni mgonjwa kushtushwa na mwanga na kelele, kupoteza fahamu na mwisho hupatwa na mauti.
Kwa mujibu wa wataalam hao, muongozo unaojitosheleza wa kupambana na ugonjwa huo ni pamoja na kutoa taarifa ya mnyama (mbwa au paka) anayehisiwa kuwa na kichaa na kumuangamiza haraka iwezekanavyo kabla hajasababisha madhara zaidi.
Pia watu wanashauriwa kuwachanja mbwa au paka wote kwa wakati mmoja na kuendelea kuwachanja watakaozaliwa huku wakidhibiti mbwa wanaotangatanga na kuwaua mbwa wote ambao hawajachanjwa.